SEPTEMBA 2, 2012, polisi waliua kikatili mwandishi wa habari wa kituo cha
Channel Ten, Daudi Mwangosi, katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa. Alikufa
mbele ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, wakati polisi hao
walipovamia ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kuwatawanya
wasifungue tawi la chama chao katika kijiji hicho.
Mmoja wa watu walioshuhudia tukio zima, ni mwandishi wa Tanzania Daima,
Abdallah Khamis. Ifuatayo ni simulizi ya kile alichokiona wakati polisi
wanaondoa uhai wa Mwangosi.
SIKU hiyo asubuhi tulipata taarifa kuwa Kamanda wa Polisi mkoani humo (RPC),
Michael Kamuhanda, alipanga kukutana na waandishi wa habari majira ya saa 2.30
ambapo waandishi walifika akiwemo Daudi Mwangosi.
Tukiwa katika chumba cha mikutano katika jengo la polisi Mkoa wa Iringa,
Kamanda wa mkoa huo, alifika akiongozana na maafisa wake wawili na kuanza
kutusomea taarifa ya zuio la mikutano ya CHADEMA iliyokuwa iendelee siku hiyo
baada ya kupisha zoezi la awali la sensa.
Alitusomea zuio hilo na kutuambia hata viongozi wa CHADEMA wameshataarifiwa
usiku wa Septemba Mosi. Tukamuuliza mbona taarifa za sensa zinaeleza kuwa kuna
mafanikio kwa asilimia 95 na waliobaki wanatakiwa waende kwa viongozi wao?
Akatujibu kuwa hilo ni agizo na linapaswa litekelezwe na CHADEMA.
Waandishi hawakuchoka kumuuliza maswali RPC na moja ya maswali yaliyoonekana
kumkera kamanda huyo ni lile lililotoka kwa Daudi Mwangosi kuwa mbona wakati wa
mwanzo walipozuia mikutano ya CHADEMA mkoani humo mikutano mingine ya CCM ndani
ya mkoa huo na sehemu nyingine nchini ilikuwa inaendelea.
Swali lingine la Mwangosi lilimtaka kamanda huyo kutumia busara katika hali
iliyopo kwa lengo la kuepusha maafa yanayoweza kutokea endapo angeendelea
kushikilia msimamo wake kuwa hakuna mkutano wa aina yoyote utakaofanyika.
Baada ya maswali hayo, tulimuona Kamanda Kamhanda akiwa amekunja sura kama
ishara ya kuchukizwa na maswali ya Mwangosi ambaye aliongeza swali lingine
kwamba, “inaonekana Kamanda umechukia kutoka ndani ya moyo wako” na kamanda
akajibu “ni lazima nichukie na nawachukia hawa CHADEMA kwa kuwa ninaipenda kazi
yangu na pia ninakaribia kustaafu na sitaki kustaafu vibaya.”
Baada ya hapo maafisa waliokuwa na RPC waliandika ujumbe kwenye karatasi na
wakamfikishia mkuu wao, na baada ya muda mkutano huo ulimalizika huku kukiwa na
kauli za utani wa hapa na pale kati ya waandishi wa habari na baadhi ya askari
juu ya kwenda kuripoti matukio ya siku hiyo.
Tulipokuwa nje ya jengo, Mwangosi, kwa kuwa ni mwenyeji wa mkoa huo, alikuwa
akitaniana na mmoja wa askari aliyevaa kiraia, ambaye alimwambia kuwa, “huko
hakutakuwa na kujuana na kuna uwezekano wa watu kufa.”
Mwangosi alijibu papo hapo kuwa hilo haliogopi kwa kuwa kifo ni ada ya mja
yeyote na kwamba ataogopa kama mtu atamuahidi kuishi milele.
Baada ya hapo, kila mmoja alitawanyika katika eneo lake, na majira ya saa
saba mchana baadhi ya waandishi walikutana ili kuanza safari katika Wilaya ya
Mufindi kwa ajili ya kuripoti mkutano wa ndani wa CHADEMA na ufunguzi wa
matawi.
Waandishi wa habari hao pamoja na mimi ni Godfrey Mushi (Nipashe), Olver
Motto (Star Tv), Renatus Mutabuzi (ITV), Clement Sanga (Mwananchi), Joseph Senga
(Tanzania Daima) na Tumaini Makene (Ofisa Habari wa CHADEMA).
Tulipofika katika mji wa Mafinga, tulipata chakula cha mchana kabla ya kwenda
katika Kijiji cha Nyololo, na muda wote huo Mwangosi alikuwa hajaungana
nasi.
Tuliondoka Mafinga kuelekea Nyololo huku mwenzetu Clement Sanga akiwasiliana
na Mwangosi aliyesema yuko katika basi na angeungana nasi tukiwa Nyololo.
Tulipofika pale tuliona askari wachache wakiwa wamesimama barabarani huku gari
lao moja likiwa linajaza mafuta katika kituo cha mafuta kilichopo eneo hilo.
Tukiwa njia ya kwenda Mbeya, mita kama 100 kutoka katika mji wa Nyololo,
kushoto kwetu tuliziona ofisi za CHADEMA zikiwa zimepambwa kwa bendera nyingi,
na kulia kwake tuliona magari manne ya askari waliokuwa na silaha.
Baada ya kupita eneo hilo, gari moja la polisi lilikuwa likitufuata, na hapo
tulishauriana kugeuza gari kurudi katika eneo la mji. Tulipofanya hivyo, na gari
la polisi lilisimama.
Wakati tunarudi katika eneo la mji, tuliegesha gari pembeni. Baadhi ya
waandishi wa habari waliingia mitaani kwa makubaliano kuwa baada ya dakika 10
tuwe tumerejea kwa ajili shughuli iliyotuleta - kushuhudia ufunguzi wa tawi hilo
jipya la CHADEMA.
Muda huo ulipofika, tulirejea, lakini Mwangosi alikuwa hajaungana nasi.
Baadaye tulianza kuona baadhi ya magari yakiwa na bendera ya CHADEMA yakipita
moja baada ya jingine.
Kuwasili kwa Mwangosi eneo la Nyololo
Saa 10.22 Mwangosi aliwasili kwa basi ambalo sikumbuki kama ni Hood au Abood;
na muda huo huo tukawaona askari wakiyatoa magari yao kutoka mafichoni na
kuingia upande wa kulia wa mji wa Nyololo kwenye ofisi za kata za CHADEMA.
Wakati askari wakiwa wanapita walikuwa wakisema Dk. Slaa anatokea eneo la
Wami. Waandishi wa habari wakawa wamejiandaa kwenda kwa kufuata njia hiyo.
Tuliegesha gari letu mbali. Mwangosi ambaye hakuwepo awali, akataka kuchukua
pikipiki ili awahi. Kwa kuwa muda huo nilikuwa naye, nikamsihi kuwa hana haja ya
kuingia gharama kwa kuwa gari la waandishi wa habari lipo. Akanielewa, na
tukaingia katika gari hilo, huku akiwa amempakata Oliver Motto wa Star Tv.
Tulipoenda kama mita 50 hivi, tulikutana na msafara wa CHADEMA ukiwa
unaelekea tunakotoka. Gari la waandishi wa habari na magari ya polisi
yakalazimika kukaa pembeni kuyapisha, kisha wakaungana nao kuelekea katika ofisi
za tawi za chama hicho.
Ofisi za tawi za CHADEMA katika mji huo wa Nyololo zipo mita zaidi ya 100
upande wa kushoto wa bararara ya kuelekea Mbeya. Awali polisi walikuwa
wameegesha magari yao barabarani wakati CHADEMA wakielekea katika ofisi zao.
Hakukuwa na vurugu yoyote. Ghafla kiongozi wa polisi ambaye alikuwepo pale -
tulimtambua kwa jina la Mnunka - aliwaamuru askari wake watoe ilani kwa
kunyoosha bendera kubwa nyekundu juu na kuwataka CHADEMA waondoke katika ofisi
zao. Tukapiga picha tukio hilo.
Wakati askari wakijiandaa kuwafuata wana CHADEMA katika ofisi zao, alitokea
mtu aliyevaa shuka na kujifunga kitambaa kichwani ambaye baadaye alijitambulisha
kama mkuu wa upelezi mkoa (RCO), akawaamuru wenzake waende katika ‘target’
lakini wasithubutu kutumia nguvu bila amri.
Hapa ndipo tulipoanza kupata wasiwasi ni nani anatoa amri kwa kuwa yule wa
mwanzo, Mnunka alijiapiza kuwa wamechoka kuvumilia, na kwamba siku hiyo CHADEMA
watawatambua. Hata tulipomuuliza maana ya kauli ile, hakutupa jibu la
kueleweka.
Katika hali hiyo, mtu aliyejitambulisha kama ndie RCO alizungumza na viongozi
wa CHADEMA, wao wakamwambia wako katika kikao cha ndani. Yeye akasema jukumu
lake ni kuhakikisha usalama unakuwepo, na kwamba kama ni suala la kikao cha
ndani hawawezi kuzuia.
Tulitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kutoka kwa RCO ambaye alikuwa
akizungumza kwa simu na mtu ambaye baadaye ilikuja kubainika kuwa ni Kamanda wa
Polisi wa Mkoa (RPC), akawa anamueleza kuwa hali ni salama. Alituahidi waandishi
wa habari tuvute subira “kwa kuwa mwenye mkoa amewasili.”
Baada ya kuwasili kwa RPC Kamuhanda, Kamanda wa FFU, Mnunka alienda
akamnong’oneza jambo. Pale pale, Kamuhanda akaonekana kukasirika. Akaagiza
CHADEMA wasimamishe shughuli yao mara moja.
Tulitaka kujua tafsiri ya mkutano wa ndani kwa Jeshi la Polisi ni ipi, ni kwa
wahusika kukaa ndani au ni ule mkutano utakaowahusisha wanachama peke yao kama
ambavyo CHADEMA walikuwa wanasema pale. RPC akatujibu kuwa hilo halielewi na
yeye si mwanasiasa.
Baada ya maelezo hayo, waandishi wa habari tulimbana RPC kwa maswali hata
ikafikia hatua ya kamanda huyo kuanza kuwanyooshea vidole baadhi yetu, huku
alimlalamikia Mwangosi kwamba kwanini hakushiba na majibu aliyopewa tangu
asubuhi.
RPC akaniambia mimi kwamba nauliza maswali yanayopingana na mtazamo wa jeshi
hilo; akamwambia Mutabuzi kuwa anamfahamu.
Baada ya hali hiyo, CHADEMA walimaliza mkutano wao katika ofisi za tawi na
wakawa wanaelekea katika ofisi za kata. Gari lililotubeba lilikuwa nyuma ya gari
la RPC ambaye baadaye dereva wake aliendesha kwa kasi kwenda mbele kutaka kuzuia
msafara wa CHADEMA.
Lakini viongozi wa CHADEMA walikuwa wameshafika katika ofisi yao ya kata na
tukashuka kwenda kushuhudia kinachoendelea. Hapo ndipo tulimkuta Naibu Katibu
Mkuu wa CHADEMA, Zanzibar, Hamad Yusuph na viongozi wengine wakisaini katika
kitabu cha wageni.
Ghafla, RPC akatoa amri ya kuwakamata viongozi wa CHADEMA waliokuwa katika
ofisi yao. Baada ya amri hiyo, wanachama wa CHADEMA waliokuwa pale wote walikaa
chini wakinyoosha mikono juu.
Balaa linaanza kwa amri ya RPC Kamuhanda
Baada ya RPC kutoa amri hiyo, polisi walioipokea walianza kurusha mabomu ya
machozi kuelekea sehemu waliyokaa wanachama wa CHADEMA. Mabomu hayo yalirushwa
na kuumiza wengi, wakiwamo waandishi wa habari. Mimi nilipigwa na kitu chenye
kishindo, nikajeruhiwa mkono wa kushoto na sehemu ya paja la mguu wa kulia.
Jitihada za polisi kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA zilifanikiwa. Baadhi ya
watu na viongozi waliwekwa chini ya ulinzi, sisi tukiwa tunaendelea kufanya kazi
yetu ya kukusanya taarifa ili kuhabarisha umma juu ya kile kinachoendelea katika
eneo hilo.
Wakati hali hiyo ikiendelea, ofisi za kata za CHADEMA hazikuwa na mtu. Askari
wakawa wanapiga mabomu kuelekea ndani ya ofisi hiyo tupu.
Tuliendelea kupiga picha tukio hilo. Ghafla askari mmoja akamgeukia mwandishi
wa gazeti la Nipashe, Godfrey Mushi, akaanza kumpiga.
Baada ya kuona mwandishi huyo anapigwa, Mwangosi aliwasogelea askari akitaka
kujua sababu za kumshambulia mwandishi wakati yupo kazini kama ambavyo askari
hao walivyokuwa wakiwajibika.
Swali la Mwangosi likavuta askari wengine. Wakamzunguka na kuanza kumpiga kwa
marungu, mateke na ngumi. Wakati hayo yakifanyika, RPC alikuwa pale
anashuhudia.
Baada ya kuona kipigo kimekuwa kikali, Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) cha
Mafinga aliingilia kati kutaka kumnusuru Mwangosi.
Wakati Mwangosi akiwa anashambuliwa, mpiga picha wa gazeti la Tanzania Daima,
Joseph Senga, naye alikuwa katika wakati mgumu baada ya askari kumdhibiti na
kuanza kumpekua mifukoni, huku mwenyewe akijitahidi kujinasua mikononi mwao.
Mbali na mimi na Senga, muda huo hakukuwa na raia yeyote katika eneo lile,
isipokuwa Godfrey Mushi wa Nipashe ambaye sina hakika kama alikuwa anafahamu
kinachoendelea maana alikuwa amepigwa sana, yuko hoi.
Baada ya kuona kipigo kinazidi kwa Mwangosi huku Senga akiendelea kupiga
picha, uzalendo ulinishinda, nikaamua kumfuata Kamanda wa Polisi mkoani humo
aliyekuwa mita zisizozidi kumi ndani ya gari lake, akishuhudia tukio lile.
Nikamuomba asaidie kumnusuru Mwangosi na kipigo kile.
RPC alishusha kioo cha gari lake, akaniangalia, kisha akafunga kioo, huku
dereva wake akawa anapiga honi. Sikujua maana ya honi hiyo.
Baada ya kuona hakuna msaada wowote kutoka kwa RPC, nilisogea karibu kwa
ajili ya kuendelea kupata picha ya tukio, ili umma ujue juu ya madhila
yanayowapata waandishi wa habari mikononi mwa polisi.
Wakati nikiwa naendelea kuchukua picha, nilimwona askari mmoja akinyoosha
mkono juu na mwingine aliyevaa kiraia akiwa ameshika bastola yake kuelekeza juu,
huku wengine wakiwa wanaendelea kumpiga Mwangosi aliyekuwa anajitahidi kuinuka
kwa kumshika mmoja wa askari wale.
Katika harakati za Mwangosi kujinasua, nilimshuhudia mmoja wa wale askari
akiwa kama anainama akaelekeza mtutu wa bunduki usawa wa tumbo la Mwangosi
aliyekuwa katika hali ya kutaka kusimama huku akipiga kelele “msiniuee,
msiniuee…”
Mara nikasikia mlipuko mkubwa pale pale walipo; baadhi ya nyama zikarushwa na
kutapakaa, nyingine zikanirukia mimi na kuchafua fulana yangu.
Kumbe walikuwa wamemlipua Mwangosi! Nikapiga picha ya mwili uliosambaratika
na kukatika vipande vipande. Nikaona askari wale wanambeba askari ambaye naye
alijeruhiwa na mlipuko uliomuua Mwangosi. Nikakimbia kujinusuru na askari
wale.
Sikuona tena usalama wangu mbele ya polisi wake. Sikumwamini tena RPC kama
angeweza kulinda maisha yangu. Nikatimua mbio kuelekea nisipopajua.
Nikiwa nakimbia nilichomoa kadi ya kamera kutoka katika kamera yangu ili
nisipokonywe. Hapo ndipo nilipokutana na mwandishi mwingine, Francis Godwin,
nikamwambia asielekee nilikokuwa natoka mimi – ambako ndiko alikuwa anataka
kwenda - kwa kuwa Mwangosi ameshauawa na polisi!
Wakati naachana na Godwin, nilichukua simu yangu na kumpigia Mwenyekiti wa
Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, ambaye ndiye Mhariri Mtendaji wa gazeti
hili kwa ajili ya kumpa taarifa. Bahati mbaya simu yake haikupokelewa.
Nikamfuata Makene (Tumaini, afisa habari wa CHADEMA) aliyekuwa amejikinga
katika gogo, alikokuwa pamoja na Oliver Motto, nikawaambia eneo hili halitufai
watatuua. Ndipo nikampigia simu Bakari Kimwanga, mwandishi wa gazeti la
Mtanzania, nikamfahamisha kuwa Mwangosi ameuawa na polisi. Tukakimbilia porini
kujificha, kila mtu akiwa analia kivyake.
Baada ya kukaa porini kwa muda, tuliamua kubadilisha nguo zetu ili
tusitambulike kirahisi. Tukatoka mafichoni kuangalia hali ya usalama. Tukaanza
kuwatafuta wenzetu ambao tulipoteana nao. Baadaye tulikodi teksi kuwafuata
wenzetu ambao wakati huo walishakimbia kutoka eneo hilo la hatari.
Tukiwa katika hoteli ya MR mkoani Iringa, mwananchi mmoja alikuja kutueleza
kuwa alifanikiwa kukusanya sehemu ya mwili wa marehemu Mwangosi pamoja na mabomu
yaliyoachwa katika eneo la tukio na walipoangalia wakaona ni sehemu ya nyama ya
utumbo iliyowekwa katika mfuko pamoja na mabomu ya machozi na kuyapanga yale
mabomu juu ya meza ya hoteli hiyo na kuyapiga picha huku utumbo wa Mwangosi
ukiendelea kuwa katika mfuko uliowekwa.
Hadi sasa sijajua endapo sehemu hiyo ya utumbo ilizikwa usiku ule mkoani
Iringa au uliunganishwa na sehemu nyingine ya mwili wake uliotawanywa na bomu
hilo kiasi cha kushindwa kujua kama ni mwili wa binadamu au ni ng’ombe
aliyechinjwa tayari kwa mauzo.
Hivi ndivyo tulivyompoteza mwandishi mwenzetu, Daudi Mwangosi, akiwa mikononi
mwa polisi
Source: www.wanabidii.net
|
No comments:
Post a Comment