Unyonyaji
wa ‘wamjini’ dhidi ya ‘wavijijini’ – Tusisahau jambo hili
Zitto
Kabwe, Mb
Mnamo
tarehe 12 Septemba, 2012 niliandika makala iliyochapwa kwenye magazeti mawili
nchini, Raia Mwema na Tanzania Daima. Makala hiyo ‘Mafukara milioni 30,
Mabilioni 30’ ilikuwa inaonyesha namna ambavyo
mfumo wa uchumi wa nchi yetu ni wa kinyonyaji. Kwamba wakazi wa mijini
wanafaidi zaidi rasilimali za nchi kuliko wakazi wa Vijijini. Vilevile
nilieleza kuwa mfumo wa uchumi wa Tanzania ni wa kifisadi na ufisadi
unafaidisha kikundi kidogo cha watu mijini au wenye tabia za kimjini na hivyo
kukosesha huduma za msingi za wananchi wengi waishio vijijini. Mwanazuoni
kijana Sabatho Nyamsenda ameandika uchambuzi wake mzuri kuhusu makala hiyo kama
‘Tangazo
la Coca Cola na wito wa Zitto dhidi ya Vizito’ ambapo amejaribu kuonyesha kuwa
masikini wa mijini ni sawa tu na mafukara wa vijijini. Sikubaliani naye.
Nitatumia Azimio la Arusha kuboresha hoja yangu na pia mfano halisi wa Mwalimu
wa Kalinzi, Kigoma dhidi ya Mwalimu wa Miburani, Temeke.
Muono
wangu unathibitishwa na mambo matatu. Kwanza ni kuongezeka kwa kasi kwa tofauti
ya kipato kati ya walionacho na wasionacho ambapo sasa kuna kundi dogo la watu
ni matajiri sana na kundi kubwa sana ni mafukara sana. Nilionyesha kuwa
asilimia 30 ya Watanzania wanamiliki asilimia 75 ya Pato la Taifa. Pili,
nilionyesha kuwa kasi ya kupunguza umasikini nchini inaonekana mijini kuliko
vijijini ambapo katika kipindi cha miaka 16, umasikini wa watu wa Dar es
Salaam, kwa mfano, umepungua kwa asilimia 12 wakati umasikini vijijini
umepungua kwa asilimia 2 tu. Tatu, nimeonyesha kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa
vijijini ipo chini ya wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa kutokana na sekta ya
Kilimo ambayo inaajiri asilimia 75 ya Watanzania imekuwa ikikua ‘flatlining’
kwa asilimia 4 wakati Uchumi wa nchi umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia 7
katika muongo mmoja uliopita.
Nilionyesha
kuwa tabaka la chini la watu wa mijini ni masikini kwani wamepewa fursa za
kuweza kuondokana na umasikini wakati watu wa vijijini ni mafukara kwani mfumo
kwa makusudi umewanyima fursa. Kimombo ninasema watu wa tabaka la chini la
mijini ni ‘poor’ na watu wa vijijini ni ‘impoverished’. Azimio la Arusha
limeonyesha muono kama huu na lilionya kutosahau mwono huu katika andiko lake.
Ninanukuu.
"Vile
vile mkazo wa fedha na wa viwanda unatufanya tukazanie zaidi maendeleo ya
mijini. Tunatambua kuwa hatuwezi kupata fedha za kutosha kuleta maendeleo
katika kila kijiji na ambayo yatamfaa kila mwananchi. Tunajua pia kuwa hatuwezi
kujenga kiwanda katika kila kijiji ili kisaidie kuleta maendeleo ya fedha na
viwanda katika kila kijiji; jambo ambalo tunajua kuwa haliwezekani. Kwa ajili
hiyo, basi, fedha zetu huzitumia zaidi katika miji na viwanda vyetu pia
hujengwa katika miji. Na zaidi ya fedha hizi huwa ni mikopo. Japo zijenge
shule, hospitali, majumba au viwanda ni fedha za mikopo. Hatimaye lazima
zilipwe.
Lakini
ni dhahiri kwamba haziwezi kulipwa kwa fedha zinazotokana na maendeleo ya
mijini au maendeleo ya viwanda. Hazina budi zilipwe kwa fedha tunazopata
kutokana na vitu tunavyouza katika nchi za nje. Kutokana na viwanda vyetu hatuuzi
na kwa muda mrefu sana hatutauza vitu vingi katika nchi za nje. Viwanda vyetu
zaidi ni vya kutusaidia kupata vitu hapa hapa ambavyo mpaka sasa tunaviagiza
kutoka nchi za nje. Itapita miaka mingi kabla ya kuweza kuuza katika nchi za
nje vitu vinavyotokana na viwanda vyetu. Kwa hiyo ni dhahiri kwamba fedha
tutakazotumia kulipa madeni haya ya mikopo ya fedha kwa maendeleo na viwanda
mijini hazitatoka mijini na wala hazitatokana na viwanda. Zitatoka wapi, basi?
Zitatoka vijijini na zitatokana na KILIMO. Maana ya ukweli huu ni
nini? Ni kwamba wale wanaofaidi maendeleo yanayotokana na fedha
tunazokopa sio kwa kweli watakaozilipa. Fedha zitatumika zaidi katika
miji lakini walipaji watakuwa zaidi ni wakulima.
Jambo
hili linafaa kukumbukwa sana,
maana kuna njia nyingi za kunyonyana. Tusisahau hata kidogo kwamba wakaaji wa
mijini wanaweza wakawa wanyonyaji wa jasho la wakulima wa vijijini. Hospitali
zetu kubwa zote ziko katika miji. Zinafaidia sehemu ndogo sana ya wananchi
wa Tanzania. Lakini kama tumezijenga kwa fedha za mkopo walipaji wa mkopo huo
ni wakulima, yaani wale ambao hawafaidiwi sana na hospitali hizo. Mabarabara
ya lami yako katika miji, kwa faida ya wakaaji wa mijini na hasa wenye
magari. Kama mabarabaraba hayo tumeyajenga kwa fedha za mikopo walipaji ni
wakulima; na fedha zilizonunua magari yenyewe zilitokana na mazao ya wakulima.
Taa za umeme, maji ya mabomba, mahoteli na maendeleo mengine yote ya kisasa
yako zaidi katika miji. Karibu yote yametokana na fedha za mikopo na karibu
yote hayana faida kubwa kwa mkulima, lakini yatalipwa kwa fedha zitakazotokana
na jasho la mkulima.
Tusisahau
jambo hili.
Japo tunapotaja unyonyaji hufikiria mabepari, tusisahau kuwa bahari ina samaki
wengi. Nao hutafunana. Mkubwa humtafuna mdogo na mdogo naye humtafuna mdogo
zaidi. Katika nchi yetu twaweza kugawa wananchi kwa njia mbili. Mabepari na
Makabaila upande mmoja; na wafanyakazi na wakulima upande mwingine. Pia twaweza tukagawa wakaaji wa
mijini upande mmoja na wakulima wa vijijini upande mwingine. Tusipoangalia
tutakuja kugundua kuwa wakaaji wa mijini nao ni wanyonyaji wa wakulima.” Azimio la Arusha,1967. (msisitizo ni wangu).
Azimio
la Arusha limerudia zaidi ya mara moja “Tusisahau jambo hili” ama “Jambo hili
linapaswa kukumbukwa sana”. Tumesahau jambo hili. Licha ya kwamba sisi
wanasiasa wa kisasa tunaona Azimio la Arusha ni nyaraka “outdated” ipo siku tutakumbushwa
kwa njia ambayo hatutakuja kuisahau. Sitaki tufike huko. Mwangwi wa “tusisahau
jambo hili” lazima uendelee kutuonyesha kuwa kuna kazi ya kufanya kuhusu
Mafukara milioni thelathini wanaoishi kwenye vijiji vyetu. Watanzania hawa wa
vijijini hawana fursa za barabara, maji, umeme na hata huduma za jamii kama
wenzao wa mijini.
Nitatoa
mfano mmoja kuonyesha tofauti ya Masikini wa mjini na Fukara wa kijijini.
Wakati nachaguliwa kuwa mbunge wa Kigoma Kaskazini (jimbo la vijijini) mwaka
2005, ilikuwa inamgharimu Mwalimu wa Shule ya Msingi Kalinzi shilingi 15,000
kwenda Kigoma mjini kuchukua mshahara wake katika Benki ya NMB kila mwezi.
Mwalimu wa shule ya Msingi Miburani, Temeke atatumia shilingi 600 tu kwenda
kuchukua mshahara wake katika Benki ya NMB tawi la Bank House (angeweza
kutembelea kwa mguu kwenda tawi la Temeke pia lakini tuchukulie alikuwa na kazi
mjini vilevile). Hawa ni walimu ambao ni daraja moja, wanalipwa mshahara sawa
lakini uwepo wa barabara (zilizojengwa kwa jasho la mkulima wa kahawa wa
Kalinzi) unampa unafuu huyu masikini wa Temeke, Dar es Salaam na kumkandamiza
katika ufukara Mwalimu wa Kalinzi, Kigoma. Mwaka 2010 barabara ya lami ilifika
Kalinzi. Barabara kubwa ya kwanza mkoani Kigoma toka Uhuru mwaka 1961. Hivi
sasa Mwalimu wa Kalinzi anatumia shilingi 3,000 kwenda Benki. Ahueni kubwa sana
ambayo walimu wengi maeneo vijijini bado hawana. Ahueni aliyosubiri miaka 40
kuipata.
Ukiangalia
Bajeti ya Tanzania utaona namna ambavyo rasilimali kubwa ya nchi inatumika
kutatua changamoto za watu wa mijini na hasa Dar es Salaam. Wabunge (ambao
wengi wetu tunatumia muda mwingi sana Dar es Salaam) bila kujali majimbo au
mikoa yao hukasirikia sana, kwa mfano, foleni Dar es Salaam na kuisukuma
Serikali kutenga fedha zaidi za kujenga barabara za Dar es Salaam. Sasa Dar es
Salaam, kwa kutumia mabilioni ya fedha, zinajengwa barabara za kupaa juu
(flyovers). Umeme ukikatika Dar es Salaam, waandishi wa habari wanaandika ‘nchi
gizani’ bila kujali kuwa Watanzania wa Urughu kule Iramba na wengine
asilimia 83 ya Watanzania wapo kwenye giza la kudumu. Zaidi ya fursa
walizonazo, masikini wa mijini pia sauti zao zinasikika. Mafukara wa Vijijini
nadra kuwasikia.
Tusisahau
jambo hili. Azimio lilisema.
No comments:
Post a Comment