Thursday, September 13, 2012




Mbunge wa Ubungo(CHADEMA)Mheshimiwa John Mnyika
---
Tarehe 9 Septemba 2012 baadhi ya vyombo vya habari viliandika habari kwamba wakazi zaidi ya 500 wa eneo la Ubungo Darajani karibu na Riverside wanalalamika kuishi kwenye mfereji wa maji taka wenye mafuta ya mitambo na mchanganyiko wa kemikali kadhaa zinazodaiwa kuzalishwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO).

Sijaridhika na majibu yaliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Felichism Mramba kwamba shirika hilo limedhibiti mfumo wa maji taka na haihusiki na tatizo hilo la kuchafua makazi na mazingira.
Kufuatia kauli hiyo, natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kutoa majibu ya wazi kwa wananchi ni kampuni gani hasa inahusika na uchafuzi huo wa mazingira na kuchukua hatua zinazostahili kurekebisha mfumo uliopo.

Ikiwa hatua hazitachukuliwa nitaungana na wananchi kufikisha malalamiko yao kwenye mamlaka zinazohusika na usimamizi wa mazingira katika Manispaa ya Kinondoni na katika Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Waziri wa Nishati na Madini na Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO watoe majibu ya wazi kwa wananchi ni lini fidia ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo itaanza kulipwa katika mwaka wa fedha 2012/2013 kutokana na kiasi cha shilingi bilioni 10 ambacho tayari kimeshaingizwa kwenye bajeti.

Izingatiwe  kwamba tarehe 04 Aprili 2012 nilifanya mkutano na wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga zaidi ya 500 katika kata ya Ubungo ambapo pamoja na mambo mengine nilitoa siku tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO kueleza hatua walizochukua katika kutekeleza ahadi waliyoniahidi  kwa nyakati mbalimbali kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 wakati wa vikao vya kamati ya nishati na madini nilipohoji kuhusu hatma ya wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi jirani na mitambo ya umeme ikiwemo kuhusu uchafuzi wa mazingira unaoendelea.

Ikumbukwe kwamba mwaka 2004 baada ya mitambo kulipuka serikali iliahidi kuwalipa fidia wananchi husika na kuwahamisha, mwaka 2009 Serikali ikarudia tena ahadi hiyo lakini mpaka tarehe 4 Aprili 2012 ilikuwa haijatekelezwa hata kwa mtu mmoja.

Ndani ya siku hizo tatu, TANESCO ilitoa ahadi ya kuwa suala la fidia kwa wananchi litaingizwa katika bajeti ya serikali mapema iwezekanavyo na tayari kiasi cha shilingi bilioni 10 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kulipa fidia ikiwa ni sehemu ya  Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme Katika Jiji la Dar es salaam (Kasma 3154).

Ili kuhakikisha kwamba mpango wa kulipa fidia ikiwa ni sehemu pia ya kuboresha mazingira ya eneo husika tarehe 27 Julai 2012 katika hotuba yangu bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani niliitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze iwapo kiasi cha 10,000,000,000 kilichotengwa kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo kitatosha kukamilisha kazi hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha uwezekano wa gharama kuongezeka kutokana na riba ya kuchelewa kufanya malipo kama ilivyotokea kwa miaka iliyopita.

John  Mnyika (Mb)
09 Septemba 2012

No comments:

Post a Comment