Rais na Amiri Jeshi
Mkuu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akitoa pole kwa mjane na ndugu wa wa Meja Jenerali
Mstaafu Anatoli Kamazima leo nyumbani
kwa marehemu Tegeta, Dar es salaam. Marehemu Kamazima, ambaye amefariki dunia usiku
wa kuamkia leo Jumatano ya Tarehe 26
Septemba, 2012 utokana na mshtuko wa moyo, alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU.
Rais Kikwete akiongea na
Brigedia Jenerali Mstaafu Tindamanyire, ndugu wa hayati Meja Jenerali
Mstaafu Anatoli Kamazima, leo nyumbani kwa marehemu Tegeta, Dar es
Salaam. Kulia kwa Rais ni Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange na
Mnadhimu Mkuu, Luteni Jenerali, Samwel Albert Ndomba. Marehemu
Kamazima, ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano ya
Tarehe 26 Septemba, 2012 kutokana na mshtuko wa moyo, alikuwa Mkurugenzi
Mkuu wa kwanza wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini
(TAKUKURU).Picha na IKULU
---
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za pole Mkuu wa
Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange kufuatia kifo cha Meja Jenerali
Anatory Ruta Kamazima (Mstaafu) aliyefariki jana tarehe 25 Septemba,
2012 katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Nimepokea
kwa mshituko na huzuni nyingi habari za kifo cha Meja Jenerali
Kamazima, ni pigo kubwa sana kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)
na Taifa kwa ujumla” Rais amesema katika salamu hizo.
Mchana wa leo Rais ameitembelea familia ya marehemu nyumbani kwao Tegeta kuwafariji wafiwa.
Marehemu
alizaliwa mwaka 1946 katika kijiji cha Maruku, Mkoani Kagera. Alijiunga
na Jeshi mwaka 1967, mara baada ya kuhitimu Chuo Kikuu mwaka 1966.
Marehemu
Kamazima amesoma kozi mbalimbali za kijeshi hapa nchini na nchi za
China, India, Uingereza na Misri na kulitumikia Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) katika ngazi mbalimbali ambapo mwaka 1989, aliteuliwa
kuwa Mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia Rushwa Tanzania, hadi alipostaafu
Juni 2003.
Rais amemuelezea marehemu Kamazima kama mzalendo na
mtu aliyeipenda na kuitumikia nchi yake kwa weledi mkubwa, uaminifu na
moyo mmoja.
“Nimemfahamu Marehemu
kwa miaka yote ya utumishi wake jeshini na serikalini kama mzalendo,
muaminifu na mwenye moyo wa kulinda nchi yake wakati wote” amesema “Marehemu Kamazima alikua mtu wa kutumainiwa sana katika nchi yetu na kamwe hatutamsahau kwa utumishi wake uliotukuka”.
“Tutamkumbuka
na kumuenzi siku zote, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa yote na
tunamuombea mapumziko mema Marehemu Kamazima. Amina”. Rais ameongeza.
Marehemu ameacha mjane, watoto na wajukuu.
Imetolewa na:
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu.
DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment