TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
KATIKA kusimamia uongozi
unaozingatia misingi muhimu ya haki za binadamu, sheria na utawala bora, Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesisitiza msimamo wake wa kutotoa
ushirikiano kwa kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi
kuchunguza kifo cha Mwandishi wa Habari wa Channel ten, Daudi Mwangosi,
kilichotokea Septemba 2, 2012, Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa.
Msisitizo huo umekuja baada
ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo kukiandikia barua (isiyokuwa na Kumbukumbu Namba)
CHADEMA, akiomba kamati yake ikutane na viongozi wa chama Septemba 25, ili
kutafakari tukio hilo na matukio ya aina hiyo yaliyowahi kutokea hapa nchini.
Itakumbukwa kuwa Marehemu
Mwangosi aliuwawa na Jeshi la Polisi akiwajibika kwa jamii katika shughuli za
uandishi wa habari, wakati askari wa jeshi hilo walipovamia ofisi za CHADEMA
Kata ya Nyololo na kuanzisha vurugu wakati wanachama walipokuwa wakiendelea na
shughuli halali za ndani za chama.
Katika barua kwenda kwa
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, CHADEMA kimesema wazi kuwa hakiko tayari kukaa na
kutafakari juu ya kifo cha Mwangosi kama ilivyopendekezwa na kamati hiyo, kwani
haipo kwa mujibu wa sheria, huku pia ikiwa imeundwa na mtu ambaye kanuni za
msingi za utawala bora, zinamtaka awe amejiuzulu au kufukuzwa kazi, kupisha
uchunguzi huru juu ya mauaji hayo yaliyofanywa na jeshi la polisi,
linalowajibika kwake kama Waziri wa Mambo ya Ndani. Kamati hiyo pia
inawahusisha polisi ambao katika tukio hilo ni watuhumiwa namba moja.
Mbali ya kusisitiza kuwa
haiwezi kutoa ushirikiano kwa kamati ambayo haipo kwa mujibu wa sheria, CHADEMA
kimeshangazwa na kusudio hilo la Kamati ya Nchimbi kutoa mwaliko wa kutaka
kukutana na viongozi wa CHADEMA, huku ikitambua wazi msimamo wa chama hiki juu
ya uwepo wa kamati hiyo mara tu ilipoundwa.
Kutoa ushirikiano kwa
kamati ambayo haina mamlaka ya kisheria ya kuhakikisha ukweli mtupu unajulikana
na haki ionekane ikitendeka kutokana na kifo hicho na vingine vingi ambavyo
vimefanywa na Jeshi la Polisi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, kwa masuala
mbalimbali yakiwemo ya kisiasa, ni kuhalalisha uvunjivu wa haki za binadamu,
Katiba na sheria za nchi. CHADEMA haiko tayari kuona hali hiyo ikifanyika.
Katika kuonesha msisitizo
wa kutokubali mwaliko wa Kamati ya Nchimbi inayotaka kutafakari matukio ya
vifo ambapo Jeshi la Polisi limewanyang’anya watu wasio na hatia haki ya
kuishi, katika barua yake ya majibu, CHADEMA pia kimeambatanisha nakala ya
barua ya tarehe 10/09/2012 iliyowasilishwa kwa Rais, ili kamati hiyo iweze
kuelewa msimamo mpana wa chama kuhusu mauaji ya kisiasa yanayofanyika nchini.
Kwa taarifa hii, CHADEMA
kinaendelea kusisitiza maazimio ya Kamati Kuu ya Chama, ambayo pamoja na mambo
mengine, iliazimia kuwa kutokana na mfululizo wa matukio ya mauaji ya kisiasa
yanayofanywa na Jeshi la Polisi katika shughuli halali za chama, Waziri wa
Mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, Mkuu
wa Operesheni wa Jeshi la Polisi Paul Chagonja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Faustine Shilogile wawajibike kwa kujiuzulu au Rais awawajibishe kwa
kuwafukuza kazi ili wapishe uchunguzi huru na wa haki.
Pia Kamanda wa Polisi
Iringa, Michael Kamuhanda, Kamanda wa FFU Mkoa wa Morogoro, na askari wote
wanaoonekana kwenye picha wakiwa wamemzunguka Mwangosi muda mfupi kabla
hajalipuliwa na kuuwawa, wakamatwe haraka na kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma
za mauaji ya Mwangosi. Kinyume na hapo ni kuchezea akili za wapenda haki na
uwajibikaji, ikiwa moja ya misingi ya amani Tanzania na dunia nzima kwa ujumla.
CHADEMA inapenda kusisitiza
kuwa itatoa ushirikiano kwa chombo kitachoundwa kwa mujibu wa Sheria huku
ikitilia msisitizo wito kwa Rais kuunda Tume ya Kimahakama/Kijaji kuchunguza
vifo vyote vyenye utata na vinavyohusishwa na masuala ya kisiasa kama
tulivyopendekeza kwake hapo kabla.
Imetolewa leo Septemba 24,
2012 Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Habari wa CHADEMA
No comments:
Post a Comment