Monday, September 17, 2012

Machafuko mapya Tana River Kenya

Machafuko Tana River
Nyumba 20 zimeteketezwa moto leo asubuhi na watu wasiojulikana katika eneo la Tana River nchini Kenya ambako kumekuwa na mapigano ya kulipiza kisasi katika siku za hivi karibuni kati ya jamii zinazoishi huko.
Kufuatia tukio hilo polisi wamewakamata watu 19 huku wakiendelea na harakati za kuwapokonywa wananchi silaha.
Ripoti kutoka katika eneo Tana Delta zinaarifu kuwa tukio hilo la kutetekeza nyumba lilitekelezwa saa kumi na mbili asubuhi na watu wasiojulikana katika vijini vya Ozi, Kipini na Bura.
Hatua hii inajiri wakati maafisa wa polisi wameanza shughuli ya kuwapokonya silaha ndogo ndogo waakazi wa maeneo hayo.
Katika msako wa leo asubuhi, bunduki mbili zilipatikana miongoni mwa wakaazi wa maeneo hayo..
Maafisa wa usalama katika eneo hilo walitoa amri kwa wenyeji kurejesha silaha ndogo wanazomiliki na ambazo wamekuwa wakitumia kwa mashambulizi ya wenyewe kwa wenyewe.
Hata hivyo kwa kuwa uhasama kati ya jamii hizi umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu baadhi wanahofia ikiwa kweli hatua ya kuwataka wenyeji kurejesha silaha huenda ikamaliza tatizo la silaha zilizozagaa miongoni mwa wenyeji wa eneo hilo, ikizingatiwa kuwa hofu ingali imetanda miongoni mwa wenyeji kufuatia machafuko yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 100.
Na pia inahofiwa ikiwa kweli tatizo la silaha au la.
Wadadisi wanasema kuwa japokuwa serikali imechelewa kuchukua hatua ili kuzima ghasia za Tana River, inatikiwa kufanya utafiti zaidi kabla ya kutekeleza mipango hiyo ili kuweza kukadiria ufanisi wake inapojihusisha na shughuli kama hiyo.
Serikali ya Kenya ilivituma vikosi zaidi vya polisi katika eneo hilo ambalo linakaliwa na jamii za wa Orma na wapokomo.
Kadhalika bunge la Kenya lilipitisha hoja ya kuwapeleka wanajeshi katika eneo hilo kwa minajili ya kuzidhibiti jamii hizo zinazozozana hasa baada ya polisi kuonekana kushindwa nguvu . Mzozo katika eneo la Tana Delta umehusishwa na tofauti za kisiasa, maji na malisho ya mifugo miongoni mwa maswala mengine.
Source:  http://www.bbc.co.uk/swahili  



No comments:

Post a Comment