Monday, September 17, 2012

Rais wa Gambia asitisha hukumu ya kifo




Rais wa Gambia Yahya Jammeh
Rais wa Gambia Yahya Jammeh, amesitisha utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa wafungwa waliohukumiwa dhabu hiyo.
Ofisi ya rais huyo imesema hatua hiyo inafuatia wito wa kimataifa uliotaka adhabu hiyo ikomeshwe lakini ameonya kuwa usitishaji huo ni wa muda.
''Hatua itakayofuata itatategemeana na iwapo kiwango cha uhalifu kitapungua ambako usitishaji huo utakuwa wa moja kwa moja, na iwapo uhalifu utaongezeka basi hukumu hizo zitatekelezwa,'' taarifa ya rais huyo imesema, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Kiongozi huyo wa Gambia alikosolewa na jumuiya ya kimataifa mwezi uliopita alipotangaza kutekeleza adhabu ya kifo kwa wafungwa.
Wafungwa tisa waliuawa kwa kupigwa risasi kufuatia uamuzi wa rais huyo huku wengine 37 wakibakia katika orodha ya wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kifo.
Rais huyo alisema kuwa wafungwa wote arobaini na saba waliohukumiwa adhabu ya kifo wangekuwa wamekwishauawa kufikia katikati ya mwezi Septemba mwaka huu.
Utekelezaji huo wa hukumu ya kifo ulikuwa ni wa kwanza nchini Gambia iliyo maarufu kwa watalii, katika kipindi cha miaka 27, huku wanaharakati wa haki za binadamu wakisema kuwa wengi wa wafungwa hao ni wale wa kisiasa.
Umoja wa Afrika na mashirika ya kutetea haki za binadamu walipinga adhabu hiyo.
Benin ambayo ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika ilimtuma waziri wake wa mambo ya nje kwenda nchini Gambia kumuonya Bwana Jammeh kuacha kutekeleza adhabu ya kifo kwa wafungwa hao.
Siku ya Ijumaa kundi la Upinzani la Gambia liliiambia BBC kuwa lina mpango wa kuanzisha serikali likiwa uhamishoni katika nchi jirani ya Senegal katika kipindi cha siku chache zijazo.
Lengo la kundi hilo la National Transitional Council of The Gambia (CNTG) ni kuona linamaliza utawala wa ki-dikteta wa rais Yahya Jammeh.
Hukumu ya kifo ilifutwa wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo Dawda Jawara lakini ikarejeshwa tena muda mfupi baada ya rais Jammeh kunyakua madaraka mwaka 1994.

No comments:

Post a Comment