Tuesday, September 18, 2012

Msemaji Wa Boko Haram Auawa Nigeria


Jeshi nchini Nigeria linasema kuwa limemuua mtu anayeshukiwa kuwa msemaji wa kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Boko Haram.

Kwa mujibu wa jeshi hilo, wanachama wengine wakuu wa kundi hilo pia walikamatwa katika msako mkali wa jeshi uliofanywa ,mapema leo Kaskazii mwa mji wa jimbo la Kano.Kundi hilo la Boko Haram bado halijatoa kauli yoyote kuhusiana na mauaji hayo yanayodaiwa kufanywa na jeshi.

Mamia ya watu wameuawa mwaka huu pekee katika mashambulizi yaliyofanywa na Boko Haram, Kaskazini mwa Nigeria.

Inaarifiwa kuwa jeshi lilisimamisha gari lililokuwa linashukiwa kumbeba mwanachama mkuu wa kundi hilo pamoja na maafisa wengine wakuu wa kundi hilo.

Duru zinasema kuwa mmoja wa washukiwa waliokuwa ndani ya gari hilo alijaribu kutoroka lakini polisi waliweza kumpiga risasi na kumuua.

Baadhi ya watu waliokuwa ndani ya gari hilo wameambia polisi kuwa mtu aliyeuawa ni msemaji wa kundi la Boko Haram ambaye pia alikuwa anatumia jina bandia la Abul Qaqa.Jeshi la polisi linasema linafanya kila hali kuhakikisha linamtambua mtu huyo.

Chanzo: http://www.bbc.co.uk/swahili/habari

No comments:

Post a Comment