Sehemu ya Barabara ya Bagamoyo Msata iliyojengwa kwa kiwangi cha lami ambayo ujenzi wake ulizinduliwa Rasmi
NDOTO ya miaka mingi ya kujengwa kwa barabara ya Msata-Bagamoyo kwa
kiwango cha lami imetimia Jumanne, Septemba 18, 2012, wakati Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
alipoweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa barabara hiyo katika sherehe
kubwa iliyofanyika eneo la Kiwangwa.
Barabara hiyo ya kilomita 64 inajengwa na mkandarasi wa ndani ya
nchi, Estim Construction, na inagharimiwa asilimia mia na Serikali ya
Tanzania bila msaada kutoka kwa mfadhili yoyote.Akizungumza kwenye
sherehe hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania, Injinia
Patrick L. Mfugale amesema kuwa barabara hiyo inayogharimu kiasi cha Sh.
bilioni 94, ikiwa ni pamoja na fedha za fidia na kumlipa mkandarasi
mshauri, itakamilika Juni mwakani.
Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais ameweka jiwe la msingi kwenye
barabara hiyo, Injinia Mfugale amesema kuwa mkandarasi wa sasa alianza
ujenzi tokea 2010 baada ya usanifu wa barabara hiyo kukamilika na baada
ya Serikali kumtimua mkandarasi wa mwanzo wa barabara hiyo, TACOPA,
Novemba 13, mwaka 2009.Amesema kuwa mpaka sasa barabara hiyo imekamilika
kwa asilimia 65, yaani kwamba kiasi cha kilomita 36.7 tayari zimewekwa
lami na kuwa ni kilomita 23 zilizosalia na ambazo zitamalizika katika
miezi tisa ijayo.Injinia Mfugale amesema kuwa mpaka sasa Serikali
imekwishakulipa kiasi cha Sh. bilioni 56.8 ikiwa ni pamoja na fedha
iliyolipwa kama fidia kwa wananchi ili kupisha ujenzi wa barabara
hiyo.Amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo hautahusisha ujenzi wa daraja
kwenye Mto Ruvu kwa sababu usanifu wa daraja hilo ulichelewa kidogo
kukamilika hata kama tayari sasa umekamilishwa.
Akizungumza kwenye sherehe hiyo, Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John P.
Magufuli amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya ujenzi wa
kilomita 11,154 za barabara za lami zinazojengwa na Serikali ya
Mheshimiwa Kikwete.“Nataka muelewe vizuri maana ya kilomita hizi. Wakati
wa Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, tulikuwa na barabara za lami zenye
urefu wa kilomita 1,330. Kati ya Uhuru na mwaka 2005, tulijenga barabara
zenye urefu wa kilomita 6,500 na kati ya 2005 na sasa tunajenga
barabara zenye urefu wa kilomita 11,154,” amesema Waziri Magufuli.Waziri
huyo amerudia msimamo wake kuwa kamwe Serikali haitawaachia watu
wanaojenga ama kufanya shughuli katika eneo la hifadhi ya barabara bila
kuwachukulia hatua.
Naye Rais Kikwete amewaambia mamia kwa mamia ya wananchi walioshiriki
katika sherehe hizo kuwa barabara ndiyo mishipa ya damu ya uchumi wa
nchi yoyote na ndiyo maana Serikali inatenga kiasi kikubwa katika Bajeti
yake kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Amesema kuwa katika Bajeti ya
sasa, barabara zimetengewa kiasi cha Sh. trilioni 2.2 ambacho ni kiasi
kikubwa cha pili baada ya Bajeti ya elimu.Rais Kikwete amesema kuwa
pamoja na faida zake kubwa na nyingi, barabara hiyo itakuwa na
changamoto zake ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa ajali za barabara,
kuongeza urahisi wa kusambaa kwa ugonjwa wa ukimwi na hata kuvutia watu
wenye lengo la kununua ardhi kubwa ya wanavijiji ambako inapita barabara
hiyo.Rais pia ameungana na Waziri Magufuli kwa kuonya: “Kama alivyosema
Waziri, wanaoifuata barabara watavunjiwa nyumba zao na hawatalipwa,
lakini wale ambao barabara inawafuata watalipwa hata wakivunjiwa.”
No comments:
Post a Comment